clubzila |
    View all
  • Explore
  • Login
  • Getting started
0%
Hassan Mboneche

Hassan Mboneche

Active Author | Journalist

Subscribe for Free Tip
Facebook
Twitter
WhatsApp
Email
Text message
Copy link
  • 2 Posts
  • 2 Photos
  • 0 Videos
  • 0 Audio
  • 0 Files
About me

2 Likes 1 Subscriber Tanzania, United Republic of Member since 16 Jan, 2025 Tunajenga Tabasamu.

© 2025 clubzila |
  • Terms of Service
  • Privacy
  • About us
  • How it works
  • Cookies Policy
  • Support
  • Contact us
  • Blog
  • English
    English Español

Pinned Post
Hassan Mboneche
Hassan Mboneche @Mboneche5
SIMULIZI: WIVU
NA; HASSAN MBONECHE 

Mvuvi hali samaki mkubwa, anakula samaki mtamu.”

Saa mbili usiku basi liliwasili kituo cha mabasi Moshi. Kijana mwenye rika kati ya miaka thelathini na ushee akawa mmoja miongoni mwa abiria walioteremka. Hakuwa na mzigo mkubwa, ni begi dogo tu la mgongoni, nalo lilionekana kuwa na vitu vichache ndanimwe. 

Aliyaacha mazingira hayo kwa hatua fupi fupi na zenye mwendo wa taratibu sana. Safari ilionekana kumchosha. Kwani namna sura ilivyopoa, ilidhihirisha hilo.

“Braza, boda?” Alisikika mwanaume mmoja kutoka upande wa kushoto kwake, alipofikia banda fulani lililopo karibu na kituo cha polisi cha askari wa usalama barabarani. 

Banda hilo ni mahususi kwa watu kupumzika, lakini baadhi ya waendeshaji wa bodaboda wamechagua kuwa kituo chao cha kazi.

Kijana yule badala ya kuongea, alimwoneshea ishara dereva boda kwa mkono, iliyompa utambuzi wa kuhitajika huduma yake.

Dereva boda akawasha pikipiki, akamfuata.

“Nipeleke Soweto,” kijana yule alisema pindi akipanda.

Sekunde kadhaa baadaye safari ikaanza.

Iliwachukua dakika kadhaa kuwasili nyumba husika kwa maelekezo ya abiria ya kumtaka dereva atumie njia ipi. Kijana akateremka, akalipa, baada ya hapo pindi dereva boda anaondoka, kijana alipiga mwendo kwa hatua ndogondogo kuielekea nyumba iliyotawaliwa na giza.

Alipoufikia mlango, kufuli lilimpokea. Akalitingisha tingisha kwa sekunde kadhaa, halafu akatoa simu mfukoni. Alitumia muda mfupi kuperuzi, kisha akaweka simu sikioni.

Baada ya kuita kwa sekunde chache simu ikapokelewa.

“Hallo!” Ilisikika sauti ya kike kutoka upande wa pili.

“Uko wapi?”

“Nipo nyumbani mume wangu, nimelala.”

Moyo ukapiga kite kwa hasira iliyochipua maumivu.

“Nyumbani?” Kijana aliuliza kujihakikishia, huku maumivu yakitawala moyoni.

Kwa nini anadanganywa?

“Ndiyo, mume wangu. Leo tulikuwa na shughuli fulani ofisini, hivyo nimerudi jioni hii. Hapa nimechoka vibaya mno.” Akamalizia kwa sauti ya kujinyoosha.
“Mmmmh!”

“Pole kwa uchovu, na ninakutakia wakati mwema.”

“Nawe pia mu...”

Kijana akakata simu kabla mkewe hajamalizia kuongea. Akalishika tena kufuli na kulitingisha tingisha.

Kitendo hicho kilienda sambamba na kuongezeka kwa kiasi cha maumivu moyoni. Kwa nini mkewe amemdanganya?

Njia mbadala ya kufungua kufuli hakuwa nayo. Mkewe ndiyo mtu pekee ambaye ana funguo za nyumba, kwani kijana sio mkazi wa mara kwa mara nyumbani. Yeye ni mwalimu wa shule ya sekondari Kigurunyembe iliyopo Morogoro.  Ujio wake leo hii alikuwa anatoka huko.

Ataingiaje ndani?

Akazunguka nyuma ya nyumba hadi kwenye dirisha moja wapo. Nyumba yao madirisha ni ya vioo, yenye nondo kadhaa. Hivyo akaokota jiwe, akavunja sehemu ndogo ya kioo iliyomwezesha kufungua loki, baada ya hapo alisogeza upande mmoja wa kioo, akaanza kukunja nondo kwa jiwe.

Alipopata nafasi iliyompa matumaini ya kupita, hakusubiri kujaribu, alipanda dirishani, akajilazimisha kuingia.
Hakufanikiwa.

Akaendelea kupinda nondo, na zingine kuzivunja kwa mara nyingine. 

Zoezi hilo alikuja kufanikiwa mara ya tatu. Hapo ndipo aliingia ndani, kisha akafunga kioo na kuelekea chumbani kwake. 

***

Ni asubuhi ya saa moja siku iliyofuata, binti wa makamo aliteremka kwenye bajaji mbele ya nyumba ile aliyoteremka mwalimu anayefundisha shule ya sekondari Kigurunyembe siku iliyopita. Baada ya kufanya malipo aliielekea nyumba hiyo. Akafungua kufuli, aliposukuma mlango, ili aingie, mlango ukagoma kufunguka.

“Maajabu gani tena haya?” Aliwaza, huku akikazana kusukuma mlango pasi mafanikio.

“Ukisikia uchawi ndiyo huu sasa,” aliendelea kuwaza.

Akasukuma kwa mara nyingine.

“Hebu usinivunjie mlango wangu. Subiri nije kukufungulia.” Ilisikika sauti kutoka ndani, huku mchakacho wa hatua ukisikika kwa nguvu kuelekea mlangoni.

Macho yakamtoka mwanamke yule. Hali ya mwili ikabadilika ghafla. Joto likaanza kumpanda na kupelekea kutokwa na kijasho chembamba. Wakati huohuo halmashauri ya kichwa chake ilizunguka huku na kule kujiuliza alichokisikia ni kweli, au yupo ndotoni.

Hakuhitaji sauti aliyoisikia ijirudie kuthibitisha mwongeaji wa sauti hiyo ni mumewe. Aliposikia mchakacho wa komeo tayari kwa kufungua mlango, aliona cha kufia nini! Akakimbia.

Alikimbia huku akikazana kutazama nyuma kila baada ya hatua kadhaa kuona kama anafuatiliwa. Mashaka yalimtawala. Huku kumbukumbu ya mawasiliano ya mwisho usiku wa jana na mumewe yakimpa picha kwamba muda aliopigiwa, ndiyo muda ambao alikuwa amekuja.

“Lakini kwa nini hakuniambia kama anakuja?” Aliwaza, akiwa ameacha kukimbia baada ya kujihakikishia yupo mazingira salama.

Alishaifikia barabara ya Soweto inayoelekea Bonite.

Akasimama hapo kuzisimamisha bajaji. Lakini nyingi alizozisimamisha zilikuwa zimejaa. Jambo lililoibua mashaka upya asije akakutwa na mumewe.

Alipoona dakika zinakatika pasi mafanikio, ikamlazimu kufuata uelekeo wa Maimoria akakutane nazo.

Kweli!

Alipolifikia kanisa la Amani, akapata bajaji iliyokuwa tupu.

“Nipeleke Dar Street. Nauli itakuwa bei gani?”

“Elfu tatu dada’angu.”

“Sawa.” Mwanamke yule alijibu, kisha akapanda, na dereva kutia moto.

Ukomo wa safari yao ulikuwa katikati ya maeneo ya Dar Street, karibu na hoteli ya Selig. Mwanamke yule aliyejaaliwa urefu na unene wa wastani akafanya malipo, kisha akateremka. Baada ya hapo alipotelea ndani ya nyumba iliyopo mbele yake.

“He, wewe!” mwanamke aliyekuwa anahangaika kufunga mlango kwenye chumba kimoja wapo alishangaa baada ya kumwona mwanamke yule aliyemkimbia mumewe.

Akaachana na zoezi la kufunga mlango, akakaza macho kumtazama.

Mwanamke aliyemkimbia mumewe akafikia kujiegemeza ukutani.

“Kulikoni?”

“Mambo yameharibika shosti yangu.”

“Mambo gani tena? Na vipi kuhusu kazini?”

“Dah! Sijui hata nikuambie nini Rebecca rafiki yangu unielewe.”

“Ni mambo yako hayo hayo ya ndoa?”

“Naomba tuingie kwanza ndani tuongee.”

“Wewe! Mimi nimejiandaa hapa niende kazini, sasa habari gani hizi unaniletea?”

“Sina namna rafiki yangu. Huko kazini utaenda tu. Ninachotaka hapa ni ushauri wako tu.”

Rebecca akafungua mlango, wakaingia ndani.

“Mume wangu amerudi jana usiku, shosti.”

“Wewe, Suzy! Usinitanie.”

“Sikutanii. Leo asubuhi niliporudi nyumbani, ndiyo nimelibaini hilo.”

“Mmmh! Pole.”

“Ninaanzaje kupoa, wakati kila siku linaibuka jambo jipya?”

“Halafu, lini ndoa yako itakuja kukaa sawa?”

“Sina hakika kama hilo litakuja kutokea. Kwa sababu toka mara ya kwanza tunaingia kwenye ndoa, nilikuja kubaini Lugome haioni thamani yangu kwake.”
“Kivipi? Na kwa nini uliolewa kama ni hivyo?” Rebecca aliuliza. Akabadili aina ya mkao na kumkazia macho Suzy.

Hii ni simulizi iliyobeba matukio ya kweli.

Nini kitatokea?

Ungana nami katika YouTube channel kwa kupitia hiyo link hapo chini.

Usisahau ku-SUBSCRIBE.
#WivuKideoni
#FilamuKwenyeMaandishi
#tunajengatabasamu 

https://youtube.com/@hassanmboneche?si=LdGXnvujyTiD97z7

Hassan Mboneche 
Moshi
17032025

1
Facebook
Twitter
WhatsApp
Text message

Pinned Post
Hassan Mboneche
Hassan Mboneche @Mboneche5

SIMULIZI click here to unlock the post

You must subscribe to view this post.
  • 1

1
Facebook
Twitter
WhatsApp
Text message

Fill Your Details
Login with Google
or
Forgot Password?
    Don't have an account?
    Two-Step Authentication
    We have sent you a code to your email
    Resend code